Monday, 29 August 2016

Miss Kinondoni Waipa Somo Kamati Ya Miss Tanzania.

#Warembo wanaoiwakilisha Kinondoni katika kumsaka mrembo wa wilaya hiyo atakayeshiriki kwenye 'Miss Tanzania 2016', wameishauri kamati ya Miss Tanzania kuzingatia vigezo, katika kuchagua mrembo ambaye ataiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia.

#Akizungumza na East Africa Radio mmoja wa warembo shiriki wanaowania taji hilo, Hafsa Mahamood, amesema ni jukumu la kamati kufanya maamuzi mazuri kwenye kumchagua mrembo wa Tanzania, ili aweze kuingia kwenye ngazi ya Taifa na kuweza kufanya vizuri kwenye ngazi ya urembo wa dunia. "Nawashauri katika kumpanga mrembo ambaye ataenda kushiriki 'Miss World' kwanza waangalie vigezo vyote ambavyo anatakiwa awe navyo, pili watende haki wasiangalie tu labda mtu mrefu sana, waangalie uelewa kwa sababu miss lazima awe na uelewa.

#Aidha, pia wanapomchagua anayeenda kuwakilisha 'Miss World', wamuandae vizuri, maandalizi ya kutosha ambayo yatamfanya yule miss kuwa na confidence", Alisema Hafsa Mahamood. Hafsa amesema kutokuwa na maandilizi mazuri kunasababisha mtu kukosa kujiamini na hatimaye kufanya vibaya kwenye mashindano makubwa kama miss world. Shindano la Miss Kinondoni linatarajiwa kufanyika usiku wa tarehe 2 Septemba 2016, ambapo walimbwende zaidi ya 20 watapata fursa ya kulipigania jukwaani taji hilo, na hatimaye kuingia kwenye ngazi ya 'Miss Tanzania'.

© 2016, Sir Lalian Mwittah Nyalali.

No comments: