Tuesday, 23 August 2016

Siri Ya Mapenzi.

Mnapokuwa katika mahusiano, kila mmoja huwa na tabia zake, kikubwa kinachofanyika ni ninyi wawili kuchanganya tabia zenu na kutoka na tabia moja ambayo itakubalika miongoni mwenu. Kupitia mtakayoyaamua kwa pamoja kuwa yanafaa au hayafai, ndiyo yatakuwa yakiongoza uhusiano wenu. Lakini kwa ujumla kuna tabia ambazo wanawake hawazipendi, hili wala huhitaji kuwa mwanasayansi wa roketi kuweza kuligundua. Huenda tabia hizi zisiwe kwa wanawake wote lakini asilimia kubwa hawazipendi. Kama kuna ambayo tutakuwa tumeisahau unaweza kuiongezea kupitia kisanduku cha maoni.

Usijifanye unajua yeye anataka nini. Kuna wakati mwanamke anaweza kuwa na tatizo, lakini shida yake sio kwamba anataka ufumbuzi wa tatizo hilo lakini anataka kuliongelea tu alafu anakuwa sawa. Kwa vile mwanaume hapendi kumuona mpenzi wake akiwa katika hali ya unyonge, yeye atakimbilia kutafuta suluhisho la tatizo badala ya kukaa na kumsikiliza mpenzi wake yakaisha. Kwa kuhangaika kwako, mtaishia kugombana maana utamkwaza zaidi. Inashauriwa uulize kwanza, ujue kama anataka suluhisho la tatizo ama anataka kulizungumzia tu tatizo alafu anakuwa sawa.

Usiwe tu unasikia, hakikisha unasikiliza kila neno analolisema. Mwanamke anaweza kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Unaweza kukuta anapika, anasikiliza muziki, mara anacheza na kazi nyingine. Lakini hali haiko hivyo kwa wanaume, wao mara nyingi akifanya jambo moja akili yake huwa katika lile jambo analolifanya. Sasa hii wakati mwingine ni mbaya kwa sababu kama wewe utakuwa unafanya kitu alafu mpenzi wako anakusemesha na wewe akili yako hata huelewi anasema nini mtaishia kugombana. Mwanamke anapenda kujua kuwa unamsikiliza na unamuelewa, tena ikiwezekana umueangalia kabisa. Hivyo kama wewe unajijua kuwa huwezi kufanyaa kazi huku unamsikiliza mpenzi wako, ni vyema mkiwa na jambo la kuzungumza mkakaa chini na kuongea kisha mkimaliza ndio muendelee na shughuli zenu.

Usithubutu kuzungumzia uzito wake. Mara zote tukiwa katika mahusiano tunategemea wapenzi watupende jinsi tulivyo, na inauma sana mtu unayejua anakupenda anapoanza kukukosoa. Mwanamke anafahamu kabisa kwamba sasa hayupo kama mwanzoni, anajua kabisa ameongezeka uzito, na kitu cha mwisho atakachotaka kutoka kwako ni wewe kumkumbusha kuwa ameongezeka uzito. Ni vyema ukatumia njia mbadala kuelezea lengo lako, mfano, mpenzi wangu nadhani tujiunge na klabu ya mazoezi, au unaweza kununua vifaa vya mazoezi vyako vya vyake ukamwambia awe anakupa company ukifanya mazoezi, na uwe unamuandalia chakula anapokuwa yupo busy ili aache kununua vyakula njiani.

Usilalamike anapokwambia ufanye kitu fulani. Ukiona mpenzi wako, zaidi ya mara tatu anakwambia fanya jambo fulani, ni vyema ukaamka hapo ulipo ukaenda kufanya hilo jambo. Mfano akikwambia bomba la bafuni linavuja zaidi ya mara tatu, jua hapo sio kwamba anadeka na usipofanya mtaishia kugombana. Kuna wakati inafika kwenye mahusiano mwanamke akikwambia naomba ufanye jambo fulani, ukimwambia nitafanya anakuuliza karne gani? ukiona hivyo jua amezoea kuwa akikwambia fanya kitu huwa hufanyi. Mwanamke anapenda akiomba kitu kifanyike, hapo yeye huwa na furaha, na kama hutakifaya, mwambie ukweli ni lini utakifanya na hakikisha unatimiza ahadi.

Usisahau kumsifia. Mwanaume anapokuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu na mwanamke humzoea kiasi kwamba kuna mambo huwa hayapi tena nafasi kama kuangalia leo mpenzi wake amevaa, anakulaje, nywele zake zikoje, kucha amebadili rangi? Wakati mwingine mwanaume hudhani, kuwa mwanamke anajua kuwa amependeza, au nywele ziko vizuri hivyo hamna haja ya kumsifia. Mwanaume hutakiwi akuacha kumsifia mpenzi wako, akija mchunguze bila ya yeye kujua, fahamu ni nini kimebadilika kwenye mwili wake, mwambie amependeza. Kama unaona utasahau, weka hata kumbukumbu kwenye simu yako ili akija ukumbuke. Na usimfike tu kwa muonekano, mwambie unavyompenda, mwambie ni namna gani atakuwa mama bora, mpe pongezi kwa kupandishwa cheo, mwambie ni kiasi gani unamthamini, usikae tu ukadhani yeye si anajua nampenda, au amependeza, hapana anataka kusikia kutoka kwako.

Usiwakodolee macho wasichana wengine. Ni rahisi sana kujua msichana huyu ni mzuri, lakini ni kosa la jinai kwa mpenzi wako kumkodolea macho msichana mwingine tena ukiwa naye. Hakikisha kuwa unaheshimu uhusinao wenu, hakikisha kuwa matendo yako yanamfanya anakuwa na uhakika kwamba anapenda na hakuna mpita njia anataka kumuibia mpenzi wake.

Usilazimishe mahaba. Kuna wanaume wao kila wakikutana na wapenzi wao akimkumbatia tu ataanza kumshika maziwa, mara mapaja mradi fujo, au umetoka kazini unamkuta anapika unaanza kuingiza mkono kwenye sketi yake. Huenda unafanya kwa nia njema lakini sio kila mara anataka. Wakati mwingine mnaweza kuufurahia uhusiano wenu mkipiga stori, mkitembea. Mwanaume yeye hupenda kuguswa kutoka nje kuleta hali ya mahaba kati ya wapenzi, lakini mwanamke anapenda mguso wa ndani ili kuweza kuamsha mshawasha wa mahaba. Sasa badala ya kuja na kuanza kumvuta, mletee zawadi, muulize untaka umsaidie nini, mpikie, kwa haya mwenye mahaba utayaona.

No comments: